Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya elimu Sekondari hususan ni shule za Busagara na Kumgogo zilizopo halmashauri ya Tandahimba kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
Mhe. Katimba amesema hayo Bungeni katika kipindi cha maswali na majibu, wakati akijibu swali la Mhe. Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe aliyeuliza “Je, lini Mabweni ya Sekondari ya Busagara na Kumgogo yatajengwa ili kuanza kidato cha Tano na Sita?”
“Mheshimiwa Spika, Mwaka 2023/24 Serikali ilipeleka shilingi 680,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Shule za Sekondari Busagara (mabweni matatu) na Kumgogo (mabweni mawili).” Mhe. Katimba.
Amesema shule za sekondari Busagara na Kumgogo zimeanza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano mwaka 2024 ambapo Shule ya Sekondari Busagara ilipangiwa wanafunzi 88 na Shule ya Sekondari Kumgogo ilipangiwa wanafunzi 93.




